MALENGA WA MOMBASA
NAKUKARIBISHA KWENYE DIWANI YANGU IITWAYO FIMBO YA KENYA.
NA ALAMIN S.SOMO
*HAYA NI BAADHI YA MASHAIRI YALIYO KWENYE DIWANI HIYO*
TANGAZO LA DIWANI YANGU
Nazuka fundi wa kale,bingwa baba wa mahoja.
Naingia na kelele,huku napija mambinja.
Malenga songani mbele,songeani kwa pamoja.
Mpate kusikiliza.
Diwani imetimia,ikamili madhubuti.
Na tena imebobea,mna tungo tofauti.
Hapa katika dunia,yaliyo kila wakati.
Na pia yaso'tokeza.
Tukuwa kitabu hiki,kwa makini na faadhi.
Ukipe na tahakiki,mahali kukihifadhi.
Kwani kina taharuki,tungo zake zina hadhi.
Kwa mbali kina mwangaza.
Katika zake nahau,msomi nikuoneshe.
Kitakutilisha kiu,kiu hiyo isiishe.
Kifanye kama ni dau,baharini kioleshe.
Kichwani kikiteleza.
Katika wako fuadi,mwenyewe ni utaona.
Vile kita'vyo buridi,utafurahika sana.
Hivyo fanya jitahidi,upate hini hazina.
Kwa kweli kinapendeza.
Upate ukitambuwe,jinsi nilivyokipamba.
Iwe ni chako mwenyewe,isiwe ni cha kuomba.
Kwa uzito wake mawe,yenye aina ya mwamba.
Pia kina maliwaza.
'Lenga na waso malenga,kwa pamoja kisomeni.
Mutapata ya muanga,yapendezayo moyoni.
Uzito mithili nanga,hewala yatukuweni.
Ndio langu kumukiza.
Beti saba zinatosha,na pawe ni ukingoni.
Utamu nilojulisha,mutautazama ndani.
Jinsi utavyo wawasha,wenyewe angalieni.
Mujuwe lakufanyiza.
Laziada naongeza,mpate mtamakani.
Mtunzi namuangaza,jina mum'tambuweni.
Ndiye mimi natokeza,jina langu Alamini.
Siwa Somo 'lonizaa.
MOLA NDIYE WAKUTUKIDHI.
Risala 'naye pendeza,kwa kazi yako njema.
Hebu na leo tokeza,nami nipate kutuma.
Upate kwenda mweleza,ni hajanelewa vyema.
Asiwe tajitatiza,atuze wake mtima.
Jmabo nililo'lengeza,nilimtaja Karima.
Mola wetu nda Muweza,ndiye wakututizama.
Yuwatulinda kwa giza,pindi linapoandama.
Na katika muangaza,pia hutulinda hima.
Fanya upate neleza,mbona wenda bima boma.
Hewa yuwatuganyiza,kwa wagonjwa na wazima.
Bila ndururu kutoza,bure huwa tunahema.
Kwa kweli hii ni jaza,Mola mwenye huruma.
Shairi nalifupiza,heri hapa nikakoma.
Na mengi ya kueleza,nakwekea ukikwama.
Ela juwa ni Muweza,wa kutukidhi daima.
3.1.2007
WALOSHIKA NI HATARI.
Mtamakani habari,uwelewao misemo.
Ingia usikithiri,ukasimame kwa kimo.
Wambe' nao kijasiri,haraka iwe kikomo.
Waloshika ni hatari,wayawate momo momo.
4.1.2007
YALIYONISWIBU
ALIF:
Angalia vyema,ninayokwambia.
Iwe muadhama,haki naumia.
Ufanye huruma,weze nirudia.
BEE:
Baa lao waja,wananifuata.
Wao wanitaja,kwakila nukta.
Nami sitofuja,kwata kutafuta.
TEE:
Tegemeyo langu,tuwe tu pamoya.
Kwenye moyo wangu,uloniachia.
Nyonda ni tewengu,kwa kunipotea.
THEE:
Thakili za moyo,zinaniumiza.
Zatia kilio,kila nikiwaza.
Lako tegemeyo,nimelipoteza.
JIM:
Jana niliota,tumelala sote.
Nikakutafuta,kwa mivungu yote.
Pendo hili tata,sijampenda yoyote.
HEE:
Hisani ya mja,kwa mja mwenzake.
Ndio yangu tija,na ikubalike.
Basi fanya kuja,naswaha ushike.
KHEE:
Kheri yangu njema,kwa nyingi salamu.
Ndio zinavuma,zinaja kwa hamu.
Mengi sitosema,nikakata hamu.
DAAL:
Daima dawamu,mimi nakupenda.
Kwa kujaa hamu,nazidi kukonda.
Usinidhulumu,niweze kuwanda.
DHAAL:
Dhana nilodhani,kwako muadhama.
Itele moyoni,yafura daima.
Fanya ihsani,ipate kukoma.
REE:
Rada ya mapenzi,huwa kali mno.
Hushusha matozi,bila ya maneno.
Ewe mpumbazi,fanya mapatano.
ZEE:
Zinduka ujuwe,nakupa yakini.
Fahamu ni wewe,uliye moyoni.
'Husu mwenginewe,mimi simuoni.
SIYN:
Sikitiko langu,wewe kukukosa.
Na ewe mwenzangu,fanya bora hasa.
Uje uwe wangu,milele kabisa.
SHYN:
Shida no'vyoona,hali kukithiri.
Tabaduli sina,siri na dhahiri.
'Shallah tukwo'nana,tayondosha nadh'ri.
SWAAD:
Swamahani sana,kama nitakosa.
Haya nalonena,yakukutakasa.
Ujuwe bayana,nyonda wanitesa.
DHAAD:
Dhahiri ya moyo,ajuwa kifuwa.
Yote kwa kituo,pia yake dawa.
Ni niwe mwenzio,naomba ridhiwa.
TWEE:
Twaja naye moyo,kwa kukutafuta.
Hivi tuko mbiyo,wapi takupata.
Ni tupe yaliyo,tutowe mafuta.
DHWEE:
Dhara ya mapenzi,ni nzito sana.
Hujawa majonzi,pia kulizana.
Kuhimili wazi,ni siwezi tena.
AIN:
Uitike mwito,niliyo kwambia.
Nyonda ni mazito,yalonilemea.
Huwa si'shi ndoto,za kujiotea.
GHAIN:
Ghafula ya mambo,yaliyo niswibu.
Yanayo makumbo,ya kunipa tabu.
Mjuzi wa tambo,fanya utiribu.
FEE:
Fasiri ya haya,na ukiitaka.
Nitakupatia,kwa unapofika.
Kwangu kunijia,ninapoteseka.
KAF:
Kadiri ya haya,ninayotamka.
Sikukudhaniya,utanitoroka.
Basi nirudiya,nipate ridhika.
QAF:
Kweli kiko mbali,nikipendacho rafiki.
Pia si sahali,mahaba ni kitu dhiki.
Yani licha wali,hata maji hayashuki.
LAM:
Lo! liwe la kuwa,kwa haya mahaba.
Kwako sitokuwa,nikatia toba.
Haki nauguwa,yazidi nikaba.
MIM:
Mato yamefura,sababu nalia.
Kutwa ni fikira,yako mazoea.
Natamani sura,zako kwangalia.
NUN:
Nina mshawasha,wako wewe umi wangu.
Huba hunipisha,ndani ini langu.
Silali nakesha,ndio kazi yangu.
WAW:
Wazo ni msiba,mithili ya nanga.
Sili nikashiba,roho yanitanga.
Kifa kwa mahaba,sitaki matanga.
HEE:
Hakika ya moyo,kwaza ndio sana.
Na katika hayo,huwa linatona.
Tozi kwa kituo,bila ya maana.
LAM-ALIF:
Lau ungejuwa,haya mambo yote.
'Ngekubali kuwa,kwangu kama pete.
Nami chanda kawa,na niskuwate.
HAMZA:
Za ndani moyoni,hasira zitowe.
Mimi sitamani,sina mwenginewe.
Hapa duniani,nakutaka wewe.
YEE:
Yamemalizika,hapa ninakoma.
Itika labeka,ewe muadhama.
Pendo la hakika,lililonivama.
WASSALAM
Wassalam nyonda,niko kituoni.
Ni dhiki kupenda,kwa umasikini.
Huwa vyanishinda,tabu siiyoni.
TAMMAT
Tamati mwishoni,hapa ninatuwa.
Jina ubaini,shika sawa sawa.
Ndiye Alamini,babangu ni Siwa.
3.1.2007mpaka
4.1.2007
SALAMU ZA WAKIBURI.
Wa kiburi nawambia,wanaopenda masifa.
Wapate kuzingatia,maneno yenye marifa.
Kunyamaza si kulia,na kulala sio kufa.
Kwani nyoka hutishia,japokuwa awe kafa.
Nawaeleza wenzangu,mupanuweni mabongo.
Kiburi ni chake Mungu,si chenu hicho kinyongo.
Tuwate hili tewengu,pia halina mpango.
Kwani sote walimwengu,asili yetu udongo.
Maneno yenye na ghashi,nawapa mupate shika.
Katika zetu aushi,tukitaka badilika.
Basi lazima tuishi,kwa atakavyo Rabuka.
Pia maisha ni moshi,ghafula yanatoweka.
Makini nawelezeto,mpate kuyatizama.
Muyafanyao ni ndoto,mwishowe huwa yazama.
Mambo hayendi kwa fito,vizuri ni kwa hekima.
Na kulia si kushoto,mbele si sawa na nyuma.
Kumbukumbu zenye puku,zinazojaa vioja.
Zitawatia shauku,siku ya Mungu ikija.
Fanyeni mtabaruku,mfanyao si ya tija.
Mjaribu kila siku,mtende yenye faraja.
3.1.2007
YAKHE HU FUNDI
Umenishangaza moyo,na kunigusa rohoni.
Kwa mambo uyafanyayo,hayangii akilini.
Sindano kweli unayo,na kushona haushoni.
Watu unawashangaza,katika wako uneni.
Uko kwenye muangaza,bado tundu huiyoni.
Uzi unakutatiza,kuingia sindanoni.
Haki nilivyo taraji,nilikuona makini.
Vipi uje kufa maji,machoni na hadharani.
Na kumbe si mshonaji,si fundi huna makini.
Kitendo ulokifanya,umetwacha mataani.
Kwa Tanzania na Kenya,bado hatujaamini.
Hata ukajibambanya,hu fundi wa cherehani.
Bora upunguze mbio,ushajitowa thamani.
Haki hu fundi wa nguo,ushoni hamfanani.
Katafute kimbilio,ushangia izarani.
Na nchi imekujuwa,mabavu unathamini.
Yako ni ya kuunguwa,yalo na nuksani.
Mazuri yenye kukuwa,si yako bwana Fulani.
Kutowa maneno hayo,hiyo si yangu imani.
Ela kwa hali niliyo,imenibidi jamani.
Nitowe kovu la moyo,lilosakama angani.
Na pia hali ilio,toweni matumaini.
Kwa wote ni hao hao,wasio mcha Manani.
Tusubiri siku hiyo,kiwanja cha hukumuni.
Nimeshafika tamati,naingia ukingoni.
Ulokalia si kiti,ni moto Jahanamuni.
Dalili hazijifiti,twazisoma vitabuni.
MWAMBIE ANAJILANI.
Haya ingia ndiani,tena uanze safari.
Urudi kwa mwafulani,kampe hizi habari.
Mwambie anajilani,kwa hakika sio siri.
Yeye kuwa ghorofani,ni amependa Suduri.
Muambie wazi wazi,usiche kusema neno.
Kwani jana sio juzi,ulimi si sawa na meno.
Kunao kushuka ngazi,hili akumbuke mno.
Afanye kama hirizi,ayawache majivuno.
Na sio yangu tabiya,kwa mimi kunena sana.
Lakini kiangaliya,imenibidi naona.
Maana anapoteya,gizani anakazana.
Tusipomzingatiya,litakufa lake jina.
Awe tunapomtaja,tumuhisi ananuka.
Kwa hilo sio faraja,ni vyema tukakumbuka.
Tumpe yenye na haja,mambo yale ya Rabuka.
Mwishoni tupate tija,siku ya siku 'kifika.
Hebu mamo yako wacha,yasokuwa na thamani.
Sijifanye umechacha,wajuwa mengi yakini.
Mwanzo ifahamu picha,uloikuta nyumbani.
Si kupangua fanicha,nawe ungali mgeni. LINAENDELEA....
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment